• Isome hapa barua ya wazi aliyo andikiwa Lady Jay Dee

    MMOJA kati ya wasanii ninaowa-heshimu sana katika muziki wa kizazi kipya kutokana na uwezo wao, ni Judith Wambura Mbibo, mwenye majina mengi ya kisanii, lakini maarufu zaidi Lady Jaydee au Jide.
    Ni bonge la msanii, anajua kuimba, anajua mashairi yanayogusa na anakwenda na wakati.

    Tokea alipojiingiza katika muziki huo zaidi ya miaka 13 iliyopita, siku zote amekuwa mtu anayepanda juu. Wamekuja wasanii wengi vijana wa kike, wamejaribu lakini hakuna kati yao aliyeweza kufikia levo zake, achilia mbali ndoto za kumpita.

    Ni kupoteza nafasi kuanza kutaja kazi za Lady Jaydee, kwa sababu zinaeleweka sana. Lakini kubwa, pengine ni kuwakumbusha tu wasomaji kwamba dada huyu aliwahi kufanya kolabo na mtu wa ndoto zake, Oliver Mtukudzi, mwanamuziki anayetamba Afrika, raia wa Zimbabwe.

    Aina ya muziki anaoufanya, Afro Pop, hauchoshi na unabadilika kadiri anavyotaka. Kwa uwezo na ubunifu wake, anaweza kuimba hata katika umri kama aliokuwa nao Bi. Kidude. Lakini kuna jambo moja ambalo kwa mtazamo wangu, ni la msingi sana kwake kulifanya kwa sasa, wakati ambao watu wanaanza kumtazama kwa jicho la maswali yanayokosa majibu. Katika maisha, siku zote binadamu ni watu wa kujifunza kwa sababu kila mmoja hufanya makosa.

    Jide anatakiwa kutazama upya nyendo zake. Ni kuhusu uhusiano na watu wake wa karibu. Nimewahi kufanya naye kazi kwa ukaribu kidogo, ni mtu mzuri, hana roho mbaya, ni mwenye kupenda kusaidia anapoweza, ni muungwana na kwa kweli, ni mwenye kupenda ushirikiano na kujituma.

    Tatizo la Jide ana hasira, kisasi na asiye makini katika matamshi yake, hasa kwa kuzingatia nafasi yake katika jamii. Historia inaonyesha ni mtu mwenye kupenda bifu zinazodumu na asiye tayari kuweka tofauti mezani kwa ajili ya mjadala wenye lengo la mapatano.

    Nina mifano kadhaa, lakini nizungumzie michache ili kushibisha hoja. Kwa tunaofuatilia Bongo Fleva kitambo, tunafahamu kwamba Jide alikuwa ‘mtoto wa Ruge’ kwa miaka mingi. Wakati wasanii wengi walikuwa wakimlalamikia Rugemalila Mutahaba, yeye alikuwa naye karibu kiasi cha wenzake kumuona kama msaliti.

    Sitaki kujua kilichosababisha wakakorofishana, lakini kauli aliyoitoa Jide kuhitimisha ugomvi wao ni kubwa na mbaya, kwamba ikitokea yeye akatangulia kufa, basi Ruge na Joseph Kusaga (Mkurugenzi, Clouds Media Group) wasifike kwenye msiba wake na endapo watakaidi, mashabiki wake wawapige mawe.

    Mtu mwenye busara, kama ambavyo Jide anastahili kuwa, hawezi kutoa kauli kama hii hadharani. Ujumbe mmoja unaoweza kuupata kwa maneno haya ni kwamba amefuta kabisa uwezekano wa suluhu, kitu ambacho siyo kizuri.

    Sugu huenda ndiye msanii aliyevutana zaidi na Ruge pengine kuliko mwingine yeyote, tena kwa miaka mingi. Tofauti kati yao zikaongezeka zaidi walipokutana tena katika ishu ya Malaria No More, lakini pamoja na machungu yote, Sugu hakuwahi kutoa kauli kali kama hii, akiamini wakati wowote mambo yanaweza kubadilika.

    Hivi karibuni Jide alitofautiana na mumewe, Gardner G Habash. Magazeti ya Global yalipoanza kuripoti juu ya kuvunjika kwa ndoa hiyo, aliyaponda sana akitoa maneno mengi ya kejeli, kitu kilichomaanisha ndoa yao ilikuwa salama. Lakini hatimaye, mwenyewe amekiri kwamba mchezo umekwisha!

    Hata hivyo, kauli yake haikuwa imekaa vizuri, pale alipokiambia kituo kimoja cha redio kwamba ‘amemuacha’ Gardner. Nia ya kauli hii ni kutaka kuuonyesha umma kwamba ni yeye ndiye aliyeamua kumtema mwenzake. Na bila shaka alifanya hivi makusudi ili kuziaminisha hisia za wengi kuwa Gardner alikuwa akimtegemea yeye, pasipo kutambua kwamba amechangia kwa kiwango kikubwa mafanikio aliyonayo.

    Na mara kadhaa amekuwa pia akitupia vijembe na kejeli kupitia mitandao ya kijamii na hata kwenye blog yake. Ninafahamiana na wasanii wanaoheshimiana naye, wanakuambia dada ni mtata!
    Najua, wote sisi kama binadamu tuna mapungufu, lakini siyo jambo baya kujiuliza na kujirudi. Kitu cha msingi sana ni kuweka akiba ya maneno, ndiyo maana hata Mfalme Suleiman alipotakiwa na Mungu kusema kitu anachohitaji kutoka kwake, aliomba apewe hekima.

    Credit GPL

  • 0 comments:

    Post a Comment

    GET A FREE QUOTE NOW

    Lorem ipsum dolor sit amet, consectetuer adipiscing elit, sed diam nonummy nibh euismod tincidunt ut laoreet dolore magna aliquam erat volutpat.