• Fahamu Matibabu ya ugonjwa wa figo

    Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikiliza, na katika kipindi chetu cha leo tunaendelea kujadili magonjwa ya figo na leo tutazungumzia ugonjwa sugu wa figo au chronic kidney disease kwa kimombo. Ugonjwa huu hutokea pale figo zinapopoteza uwezo wa kutenda kazi ambayo hutokea taratibu, na huchukua muda wa takribani miezi kadhaa hata miaka.

     Figo zinapopoteza uwezo wake wa kutenda kazi, kusanyiko na limbikizo la maji, uchafu na sumu hutokea mwilini mwa mgonjwa na pia husababisha kutokea kwa maradhi mengine kama tulivyoyataja katika vipindi vilivyopita. Lakini huenda ukajiuliza swali kwamba je, kuna tofauti gani kati ya ugonjwa sugu wa figo na kushindwa figo kufanya kazi kwa ghafla yaani Acute Renal Failure?
    Tofauti ni kwamba ARF hutokea ghafla, huchukua muda mfupi kati ya siku hadi wiki kadhaa kuwa tatizo kubwa zaidi. Tofauti nyingine ni kuwa kushindwa kufanya kazi figo kwa ghafla hutokana na tatizo linaloathiri figo moja kwa moja, mishipa yake ya damu au mtiririko wa mkojo unaotoka kwenye figo.

     Aidha ARF mara nyingi huweza kurekebishwa na mgonjwa akapona kabisa, ingawa kwa baadhi ya wagonjwa sehemu fulani ya figo inaweza isipate nafuu na ikaendelea kudorora kiutendaji.

    Hatua za Ugonjwa Sugu wa Figo: Ugonjwa sugu wa figo umegawanywa katika hatua kuu tano, kulingana na ukubwa wa tatizo. Hatua hizo zimegawanywa kulingana na kiwango cha GFR kilichofikiwa na figo husika. Glomerular Filtration Rate kwa kifupi GFR ni kiwango kinachoonesha uwezo wa utendaji kazi wa figo.

    GFR hupima uwezo wa glomeruli au chujio la figo katika kuchuja uchafu, maji pamoja na sumu nyingine kwa kila dakika moja kwa mtu mwenye wastani wa urefu wa mita mraba 1.73. Kadiri GFR inavyopungua ndivyo inavyoashiria ukubwa wa tatizo katika figo.

    Hatua ya kwanza mgonjwa huwa na GFR ya zaidi ya mililita 90 kwa dakika kwa mita mraba 1.73, ambapo madhara madogo huwepo katika figo, huku kiungo hicho kikiendelea kuchuja uchafu kama kawaida. Hatua ya pili ni pale GFR inapokuwa ya kati ya mililita 60-89 kwa dakika kwa mita mraba 1.73 na katika hatua hii, kiwango cha utendaji kazi cha figo hushuka kwa kiasi kidogo.

    Hatua ya tatu, GFR huwa kati ya mililita 30-59 kwa dakika kwa mita mraba 1.73. Katika hatua hii utendaji kazi wa figo hupungua zaidi, wakati katika hatua ya nne GFR hushuka zaidi na kuwa kati ya mililita 15-29 kwa dakika kwa mita mraba 1.73 na hapa utendaji kazi wa figo huwa wa chini mno. Katika hatua ya tano mgonjwa huwa na GFR chini ya mililita 15 kwa dakika kwa mita mraba 1.73 hatua ambayo huitwa pia kushindwa kufanya kazi sugu kwa figo au CRF neno ambalo tutalitumia zaidi kumaanisha kushindwa kufanya kazi sugu kwa figo yaani chronic renal failure.

    Wapenzi wasikilizaji, kuhusiana na wanaopatwa zaidi na tatizo hili tunaweza kusema kuwa, ugonjwa sugu wa figo ni maarufu zaidi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea.

    Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha udhibiti wa magonjwa cha nchini Marekani (CDC), ugonjwa sugu wa figo ni miongoni mwa matatizo ya kiafya yanayojitokeza kuchukua chati za juu sana nchini humo. Ripoti hiyo inaonesha kuwa karibu asilimia 17 ya watu wazima wenye umri wa miaka 20 na kuendelea wanasumbuliwa na ugonjwa sugu wa figo.

    Aidha ripoti hiyo inaonesha kuwa karibu watu nusu milioni wapo katika matibabu ya dialysis au wameshawahi kubadilishiwa figo. Mambo kadhaa yanahusishwa na ongezeko la ugonjwa sugu wa figo, miongoni mwayo ni ugonjwa kisukari, shinikizo la damu, unene na uzee. Aidha mabadiliko katika tabia na namna watu wanavyoishi pia vimeonekana kuchangia ongezeko hili kwa kiasi kikubwa. Lakini je, tatizo hili kubwa la figo husababishwa na nini?
    Visababishi vya ugonjwa sugu wa figo


    Pamoja na kwamba ugonjwa sugu wa figo hutokana na magonjwa kadhaa ambayo kimsingi yanaathiri figo yenyewe, visababishi vikuu vya ugonjwa sugu wa figo ni kisukari na shinikizo la damu. Kisukari cha aina ya 1 na ya 2 husababisha hali iitwayo kisukari cha figo au kwa kimombo diabetic nephropathy. Shinikizo la damu kama lisipodhibitiwa vyema, baada ya muda fulani husababisha madhara katika figo.

     Visababishi vingine vya ugonjwa sugu wa figo ni pamoja na magonjwa kama vile systemic lupus erythematosus pamoja na maambukizi ya bakteria jamii ya streptococci ambao husababisha madhara katika chujio la glomeruli ambayo huathiri mfumo wa uchujaji uchafu katika figo. Pia magonjwa ya kurithi ya figo kama vile Polycystic kidney disease. PKD huambatana na hali ya kuwa na vimbe ndogo ndogo zilizojaa maji (cysts) katika figo.

    Vimbe hizi hufanya figo ishindwe kufanya kazi zake sawasawa na hivyo kusababisha ugonjwa sugu wa figo. Vilevile matumizi ya kila siku ya muda mrefu ya baadhi ya madawa ya kutuliza maumivu kama vile ibuprofen au acetaminophen yanaweza pia kusababisha ugonjwa sugu wa figo.

    Hali hii huitwa kitaalamu analgesic nephropathy. Matumizi ya baadhi ya madawa kama antibiotics za aminoglycosides kama vile gentamicin pia husababisha madhara katika figo na hatimaye ugonjwa sugu wa figo.

     Kadhalika hali ya mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye figo kuzeeka, kuwa migumu kiasi cha kushindwa kutanuka na kusinyaa. Atherosclerosis husababisha upungufu mkubwa wa damu katika figo husika, kwa kitaalamu hali ambayo inaweza pia kusababisha madhara zaidi kwa figo na hatimaye ugonjwa sugu wa figo na hata CRF.

     Magonjwa kama vijiwe katika figo, kuvimba tezi dume, kuziba kwa njia ya mkojo pamoja na saratani, vyote vinaweza pia kusababisha madhara katika figo na hatimaye kusababisha ugonjwa sugu wa figo. Vyanzo vingine vya ugonjwa sugu wa figo ni pamoja na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ambayo husababisha hali inayoitwa HIV nephropathy, ugonjwa wa sickle cell unaoweza kusababisha kuziba kwa mirija inayosambaza damu kwenye figo au upungufu wa damu kwenye figo. Pia matumizi ya madawa ya kulevya, maambukizi sugu katika figo na saratani za figo.
    Vihatarishi vya Ugonjwa Sugu wa Figo

    Mtu aliye na mojawapo ya vitu au magonjwa haya ana hatari kubwa ya kupata ugonjwa sugu wa figo na hatimaye CRF. Wenye matatizo haya, hawana budi kuhakikisha kuwa figo zao zinafanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kuangalia utendaji kazi wake. Magonjwa hayo ni kisukari aina zote mbili, shinikizo la damu, kiwango cha juu cha kolestroli au lehemu katika damu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya ini, magonjwa yanayohusiana na aina mbaya ya protini (Amyloidosis), ugonjwa wa seli mundu (Sickle cell disease), ugonjwa wa mzio au mcharuko mwili wa lupus (Systemic Lupus erythematosus), magonjwa ya mishipa ya damu kama vile magonjwa ya mzio katika artery (arteritis) au vasculitis, matatizo katika njia ya mkojo ambapo mkojo badala ya kutoka nje (kushuka chini) hupanda kurudi ndani ya figo (Vesicoureteral reflux), matumizi ya mara kwa mara ya madawa ya kutuliza mcharuko mwili au mzio na kuwa na historia ya magonjwa ya figo katika familia.&&&&&&&&&&

    Wapenzi wasikilizaji figo zina uwezo wa ajabu wa kukabiliana na hali ngumu na matatizo katika utendaji kazi wake kwa muda mrefu. Kwa sababu hiyo basi, mgonjwa sugu wa figo anaweza kudumu katika hali yake kwa muda mrefu bila kuonesha dalili zozote zile.

     Dalili za ugonjwa sugu wa figo hujitokeza pale utendaji kazi wa figo unapokuwa umeshuka na kufikia kiwango cha chini kabisa.

    Dalili hizo ambazo baadhi tulizitaka katika vipindi vyetu vilivyopita ni pamoja na kukojoa sana hasa wakati wa usiku, kuvimba uso na macho, kuvimba miguu, ongezeko la shinikizo la damu, uchovu na udhaifu wa mwili kutokana na upungufu wa damu au kurundikana kwa uchafu na sumu mwilini, kupoteza hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika na mwili kuwasha, kupata michubuko kirahisi katika ngozi, na ngozi kuwa nyeupe kwa sababu ya upungufu wa damu.

    Dalili nyingine ni kupumua kwa tabu kutokana na mrundikano wa maji katika mapafu, kichwa kuuma, kujihisi ganzi miguuni au mikononi, kupata shida ya kupata usingizi au kulala usingizi wa mang'amung'amu, mabadiliko katika uwezo wa utambuzi kwa sababu ya madhara katika ubongo yanayosababishwa na mrundikano wa uchafu na sumu za urea, maumivu ya kifua kwa sababu ya mzio katika gamba la juu la moyo, kutokwa damu kwa sababu ya ukosefu wa chembe zinazosaidia damu kuganda, maumivu ya mifupa na kuvunjika kirahisi, na pia kukosa hamu ya tendo la ngono kwa wanaume.

    Daima tukumbuke kuwa miili yetu ni tunu na baraka kubwa kutoka kwa Mungu Muumba, hivyo tuilinde kwani kufanya hivyo mbali na kutuepushia matatizo, maumivu maradhi mbalimbali pia ni njia mojawapo ya kumshukuru Mungu kwa neema nyingi alizotujaalia. Hadi wiki ijayo, kwaherini.




  • 0 comments:

    Post a Comment

    GET A FREE QUOTE NOW

    Lorem ipsum dolor sit amet, consectetuer adipiscing elit, sed diam nonummy nibh euismod tincidunt ut laoreet dolore magna aliquam erat volutpat.