Mapambano hayo yalitokea katika Mapango ya Amboni yaliyopo katika Kijiji cha Mleni Majimoto, nje kidogo ya Jiji la Tanga ambapo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) nalo liliongeza nguvu kwa kupeleka wanajeshi wake eneo la tukio.
Akitoa taarifa za tukio hilo kwa waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa huo, Magalula Said Magalula, alisema chanzo chake ni baada ya majambazi kupora silaha za askari waliokuwa doria barabara ya nne jijini humo na kutokomea kusikojulikana; hivyo Jeshi la Polisi lilianza kuzisaka silaha hizo.
"Baada ya askari kupata taarifa juu ya eneo zilipofichwa silaha hizo, waliamua kwenda moja kwa moja katika eneo husika ili kuzichukua lakini baada ya kufika hali ilikuwa tofauti ndipo mapambano kati yao na majambazi yakaanza," alisema.
Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani humo, wanaendelea na jitihada za kuwasaka wahalifu wanaodaiwa kujificha katika mapango hayo na kuimarisha ulinzi mkoani humo.
"Kimsingi Tanga iko salama, tumeweka nguvu zetu katika eneo waliloficha silaha, jana (juzi), tumezunguka maeneo yote ambayo yalikuwa na majibizano ya risasi na askari wetu.
"Hawa majambazi wametokomea na kuingia katika mapango mengine, lakini jitihada za kuwasaka zinaendelea kuhakikisha tunawatia nguvuni majambazi wote," alisema Magalula.
Aliwataka wananchi mkoani humo, kuendelea na shughuli zao bila wasiwasi kwani hali ni shwari na ulinzi unaendelea kuimarishwa ili kuwadhibiti majambazi wanaohatarisha amani ya nchi.
Magalula alithibitisha kifo cha askari mmoja wa JWTZ ambaye alifariki baada ya kupigwa risasi katika majibizano na majambazi ambapo mwili wake umesafirishwa jana kwa ajili ya mazishi katika Kijiji cha Kwashemshi, wilayani Korogwe.
Aliwatoa hofu watalii na watu waliojipanga kutembelea mapango hayo akisema uhalifu umefanyika nje kidogo ya eneo la kivutio hivyo jamii isiwe na hofu yoyote juu ya Mapango ya Amboni.
Pamoja na maelezo ya Magalula, hali ya wasiwasi imeendelea kutanda miongoni mwa wananchi ambapo idadi ya askari kutoka mikoa tofauti nchini imeendelea kuongezeka mkoani humo na kwenda katika mapango hayo ili kukabiliana na wahalifu wanaodaiwa kujificha.
Baadhi ya wananchi wanalitaka Jeshi la Polisi kutoa taarifa ya kueleweka juu ya kukundi cha wahalifu (majambazi), ambao wanadaiwa kurushiana risasi na polisi, kusababisha kifo.
Siku tatu zimepita tangu kuzuka mapambano hayo kati ya majambazi, polisi na wanajeshi ambapo wananchi wengi wanaamini kuwa, hali ya usalama bado tete.
Imani hiyo ya wananchi inatokana na migongano ya kauli za Jeshi la Polisi juu ya mapambano hayo na baadhi ya silaha zilizokutwa katika mapango ambazo ni mapanga, pinde, mishale na vifaa vya kutengeneza milipuko.
Vitu vingine vilivyokamatwa ni pikipiki mbili, baiskeli tatu, mavazi ya aina mbalimbali pamoja na vyakula ambavyo vinaashiria kwamba watu hao walikuwa wakijipenyeza ndani ya jamii kutafuta huduma muhimu bila kufahamika.
"Vifaa vilivyokamatwa katika eneo la tukio ni tofauti kabisa na madhara waliyopata askari wetu waliokuwa kwenye operesheni ya kusaka bunduki zilizoporwa, baadhi ya askari wamejeruhiwa na kulazwa Hospitali ya Rufaa ya Bombo.
"Vipo viashiria vinavyoonesha hali ya ulinzi na usalama hapa Tanga haijatengemaa kutokana na hali ya mazingira kwani wahalifu waliweka makazi ndani ya mapango bila kubainika," walisema.
Waliongeza kuwa, tukio la askari kuporwa silaha aina ya SMG mbili zenye risasi 60 kwenye kibanda cha chipsi wakiwa doria ni cha fedheha.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana jioni ambazo si rasmi, zinasema Jeshi la Polisi limefanya kikao kizito cha kimkakati mkoani humo na idadi kubwa ya askari, bado wanaendelea kumiminika.
MAJIRA.. limeandika
0 comments:
Post a Comment