Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu(Uwezeshaji)Dk.Mary Nagu |
Hayo ni maneno ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Bunda mkoani Mara.
Wasira, anayasema hayo wakati akichangia mjadala, ambao Bunge limeuidhinisha kuwa sheria ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi, (sura Na. 103) ya mwaka 2014 (PPP).
“Tunapozungumza uwekezaji tuzungumzie watu wa hapa nchini, wawezeshwe ili nao wawekeze na kuiletea nchi maendeleo endelevu,” anaeleza Wasira.
Hata hivyo, Wasira anashindwa kuweka bayana namna serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Uwekezaji na Uwezeshaji, imetenga fedha kiasi gani kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji hao wa ndani.
Anashauri serikali kuanzisha mifuko ya fedha, itakayotumika kuwakopesha wawekeji wa ndani, kwenye taasisi za fedha, kama vile Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) na Benki ya Kilimo Tanzania (TAB).
Mipango hii ambayo inaelezwa na kiongozi huyu wa kitaifa, inakinzana na maelezo yaliyowahi kutolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akizungumzia uwekezaji katika uchimbaji wa gesi na mafuta.
Profesa Muhongo aliwahi kusema kwamba hakuna Mtanzania mwenye uwezo wa kuwekeza katika miradi hiyo ya gesi na uchimbaji wa mafuta ingawa wafanyabiashara wa ndani wameishaweka bayana kwamba uwezo wanao ikiwa serikali itawapa vitalu vya uchimbaji.
Muhongo anakejeli kauli za wafanyabiashara hao hao huku akisema uwezo wa uwekezaji unaishia kwenye vyombo vya habari, maandazi na juice, kauli ambayo pamoja na mambo mengine, imefifisha matumaini ya Watanzania katika kuwekeza.
Hata hivyo, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu, anatilia mkazo maelezo ya Wasira akisisitiza kuwa serikali sasa imeamua kuwezesha uwekezaji wa ndani.
Anasema marekebisho yaliyofanyika kwenye sheria ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi, yanatoa fursa kwa sekta binafsi ya ndani,kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo.Anawataka Watanzania kujitokeza kuwekeza katika sekta mbalimbali,akisema ushiriki wao katika kukuza uchumi wa taifa, hauna mjadala na haiwezekani ukapuuzwa.
“Ninasema kwa niaba ya serikali, kama kuna yeyote anayefanya hivyo,anafanya kwa niaba yake binafsi, siyo kwa niaba ya serikali,” alieleza Dkt. Nagu.
Tanzania ina rasilimali nyingi, lakini hazijaondoa taifa kwenye umaskini, hivyo ni wazi kwamba kuwa na rasilimali pekee hakutoshi,kulihakikishia taifa maendeleo kiuchumi.
“Hatuwezi kutegemea maendeleo kutoka kwa wawekezaji wa nje,kwa sababu wakighairi katika jambo moja, tutashindwa kufikia malengo, hivyo tutateteleka kiuchumi,” anaeleza Dkt. Nagu.
Anasema sheria hiyo ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi,(sura namba. 103) ya mwaka 2014 (PPP), pamoja na mambo mengine, itapunguza urasimu usiyo wa lazima ambao, unaochangia kukwamisha maendeleo nchini.
Kupitia PPP, serikali itakuwa ikitekeleza miradi yenye kuvutia wawekezaji, kwa kushirikiana na sekta binafsi, ili kufikia malengo iliyojiwekea kimaendeleo.
Miradi isiyovutia uwekezaji binafsi, mathalani huduma za umeme,mawasiliano, afya, elimu na maji hasa vijijini, serikali itajikita zaidi kuwekeza rasilimali zake.
Utekelezaji wa sheria hiyo, umetoa kipaumbele kwa wawekezaji wa ndani, matamko ya kisera, ambapo inaagizwa kujenga uwezo, kuhawilisha teknolojia na kuwezesha wananchi kiuchumi, kupitia miradi ya maendeleo.
Anasema Sera na Dira ya taifa ya Mwaka 2020/2025, inataka Watanzania kumiliki na kushiriki kikamilifu, kujenga na kusimamia uchumi wa sekta zote.
Kwa msingi huo, anasema jambo linalotakiwa kujadiliwa ni namna gani bora ya ushiriki, inayoweza kutoa wigo mpana kwa wawekezaji wa ndani, kuwekeza katika miradi ya maendeleo nchini.
Naye Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, akizungumza bungeni anatoa wito kwa Mtanzania yeyote mwenye fedha, kuwekeza kwenye reli na bandari.
Hata hivyo, akisoma maoni ya mapendekezo ya kambi ya rasmi ya upinzani bungeni, kuhusu mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2015/2016,
Mbunge wa Mbozi Magharibi mkoani Mbeya (Chadema), David Silinde, anasema serikali imekuwa ikihadaa wananchi kwamba inatekeleza ilani ya CCM na mipango mbalimbali.
Lengo la jumla la sehemu hiyo ya kwanza ya mipango ya maendeleo ya taifa, inaelezwa na mbunge huyo kuwa ni kutoa fursa ili hazina ya rasilimali za nchi, zitumike ipasavyo,
Kwa kuweka mazingira na kutanua wigo wa ukuaji wa uchumi, ili watu maskini waweze kukua kiuchumi, jambo ambalo Silinde anasema halitekelezwi ipasavyo.
Anasema mpango wowote unaotegemea fedha kutoka nje, lazima uwe na matatizo.
Anashauri utekelezaji wa miradi mikubwa, kama vile ya umeme ihusishe sekta binafsi hapa nchini, kwa serikali kuuza hisa zake.
Anasema sekta ya nishati ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi,lakini kwa kuwa inahitaji uwekezaji mkubwa imekuwa ikiweka kando wawekezaji wa ndani.
Anasema dosari hiyo imekuwa chanzo kikuu cha mapato ya mafisadi, ndani na nje ya Tanzania.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment