Dr.Hamis Kigwangwallah |
Vijana wa umoja huo kwa hivi sasa wamegawanyika vipande vipande kutokana na kutafunana ndani kwa ndani, na ukipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya wajumbe wa UVCCM ama kuwasikia, utabaini kuna mpasuko wa kimakundi.
Mpasuko huo ndani ya umoja huo unasemekana umesababishwa na baadhi ya viongozi ambao kwa sasa wanaegemea zaidi kimaslahi kupitia kwa wanasiasa wenye nia ya kuhitaji madaraka ya nchi ama wale wanatuhumiwa kwa ufisadi.
Kutokana na hali hiyo kumesababisha miongoni mwao kuwatetea viongozi mafisadi ama wale wenye mtazamo wa kuhitaji madaraka na kusahau malengo ya umoja huo ya kuwakemea wala rushwa na ‘kukinyoosha’ chama chao pale kinapoenda kinyume.
Hivi karibuni akiwa jijini Mwanza akizungumza na vijana wa umoja huo wa Chuo cha Mtakatifu Augostino jijini Mwanza, mbunge wa jimbo la Nzega, Dk. Hamis Kigwangwallah, anazungumzia jinsi umoja huo ulivyopoteza muelekeo.
Dk. Kigwangwallah anasema kwa sasa umoja huo umetekwa na makundi na kusababisha mpasuko unaohatarisha umoja huo kuyumba ukilinganisha na zamani.
Anasema umoja huo kwa sasa wamejaa vijana ‘wazandiki’ ambao wanashindwa kukemea maovu yanayofanyika hivi sasa nchini na baadhi yao wanakuwa wasemaji wa wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
“Vijana wa zamani wa umoja huu, tofauti kabisa na nyie wa sasa…hatuwezi kuulinganisha umoja wa vijana na ule wa akina John Nchimbi, John Guninita na wengineo, huu umejaa makundi ya kuwabeba wengine, kushindwa kukemea mafisadi zaidi ya kuwabeba,” anasema Dk. Kigwangwallah.
Mbunge huyo ambaye ametangaza nia ya kuwania nafasi ya urais kupitia CCM, anasema utofauti wa umoja huo umeonekana kipindi hiki ambacho nchi inakabiliwa na kashfa ya akaunti ya Escrow.
“UVCCM ulikuwa wakati wake wa kukemea jambo hili la Escrow, lakini wameliacha limetekwa na wapinzani…kazi kubwa ni kuwapo upande wa watu fulani wagombea ama mafisadi, wanashindwa kuwaiga akina Guninita na Nchimbi kweli,” anahoji Kigwangwallah.
Aidha, Dk. Kigwangwallah anasema lazima vijana wa umoja huo wabadilike sasa na kulazimisha mabadiliko katika kipindi hiki ili kuondokana na mfumo wa uongozi wazee kujitwisha madaraka.
“Lazima vijana tubadilishe mabadiliko ya kiutawala, tukikaa hivi tulivyo sasa wazee watatudharau lakini kubwa ni lazima waondoke ili kupisha kizazi cha sayansi na teknolojia yaani kile dot.com, maana mtazamo wao ni wa kizamani hawajui kama kuna mabadiliko ya teknohama,” anasema.
Anasema kwa sasa nia yake ni kuwaonyesha vijana wazalendo kuchukua uongozi wa nchi kupitia uchaguzi ujao, lakini itadhihirika katika uchaguzi wa mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma Mei mwakani.
Mbunge huyo anasema iwapo vijana wa CCM wameshindwa kuitetea nchi yao kutokana na kundi la watu wachache kuiba zaidi ya Sh. bilioni 300 za akaunti ya Escrow IPTL kwa kukaa kimya, basi nguvu zaidi inabidi kuelekezwa kwa uongozi wa vijana uchaguzi ujao.
“Mtu anaiba maslahi ya umma na kisha anatumia kivyake na familia yake, huyo hafai ndani ya chama chetu na ninashangaa kuona umoja wa vijana wetu unakaa kimya na kuwaacha watu wa namna hii wanafanya watakacho, wanatakiwa kushughulikiwa kwa ufisadi walioufanya kwa pesa za Escrow,” anaongeza kusema.
Anasema hivi karibuni watu wenye heshima zao jijini Dar es Salaam, wameonekana wanachukua pesa benki moja kwa kutumia mabegi makubwa pamoja na mifuko ya plastiki, na kuamini watu hao si salama.
Kigwangwallah anasema haingii akilini mtu kutoa pesa benki ambako ni sehemu salama na kuzihamishia sehemu nyingine ambazo si salama, hali inayotia wasiwasi kuwa si wema.
Hata hivyo, mbunge huyo anazidi kukomaa na umoja na vijana wa chama hicho (UVCCM), na kusema iwapo wangewajibika kusimamia kashfa hiyo wangeuweka umoja huo katika mstari mzuri na kuondoka katika mpasuko uliopo sasa.
Anasema, “Umoja wa vijana wangeingia mtaani na kulipinga hili, lazima wabunge wa upinzani akina David Kafululia (NCCR-Mageuzi) na Zitto Kabwe (Chadema), wasingepata nafasi ya kushupalia maana wangetekwa na hoja zao.”
“Nasikitika kuona umoja huu upo tofauti kabisa na ule wa zamani, kwani wa sasa umejaa ushabiki wa viongozi ambao haukosoi serikali pamoja na kushabikia wagombea urais wenye harufu ya ufisadi."
Anasema ni wakati wa vijana kuchangamkia nafasi za uongozi hivi sasa kwani ni muda muafaka kufanya hivyo ili kuondokana na kasumba ya kuwapa wazee kuongoza kila nafasi.
Dk. Kigwangallah ambaye ameonyesha zaidi kukerwa na umoja wa vijana wa chama chake jinsi wanavyokiuka mienendo yao, lakini anasema kubwa kwake ni kujaribu kuwaonyesha vijana nchini kwamba wana nafasi kubwa ya kuongoza nchi.
“Uongozi unatakiwa kuongozwa kisasa na vijana ambao wanaiona dunia kupitia sayansi na teknolojia kama facebook, whatsap, instragram…hawa wazee hawajui lolote hata kutumia mitandao hiyo,” anaeleza.
Anasema uongozi ni kipaji, hivyo vipaji vya namna hiyo vimejaa kwa vijana wengi nchini ambao hata hivyo wanashindwa kuvitumia kutokana na uoga hivyo kuamua kama kijana kujitosa kuwania nafasi hiyo kubwa nchini.
Dk. Kigwangwallah anasema ameamua kujitosa kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo, kwa lengo la kupambana na ufisadi ulioshamiri kwa baadhi ya viongozi waliopo madarakani.
Uchotaji wa pesa katika akaunti ya Escrow IPTL, ni moja ya sababu ambayo ‘itawaumiza’ watangaza nia wengi waliopo katika uongozi wa serikali hivi sasa kutokana na kuguswa na kashfa hiyo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment