
Viongozi wa Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe na Deo Filikunjombe wamemtuhumu Waziri
William Lukuvi kuwa alitaka kuiba ripoti ya kamati yao kuhusu uchotwaji
wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Sakata hilo lilihitimishwa Jumamosi
wakati Bunge lilipoazimia kuwajibishwa kwa watu wote waliohusika kwenye
uchotwaji wa fedha hizo, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za
kisheria kwa taasisi za fedha zilizoruhusu kufanyika kwa miamala mikubwa
kinyume na taratibu za kibenki.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao wawili kutoka Chadema na CCM walilieleza gazeti la Mwananchi kuwa jaribio hilo lilishindikana baada ya wao na mjumbe mwalikwa, Luhanga Mpina (CCM) kuamua kukesha wakiilinda ripoti hiyo tangu ilipokuwa ikichapwa hadi ilipowasilishwa bungeni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao wawili kutoka Chadema na CCM walilieleza gazeti la Mwananchi kuwa jaribio hilo lilishindikana baada ya wao na mjumbe mwalikwa, Luhanga Mpina (CCM) kuamua kukesha wakiilinda ripoti hiyo tangu ilipokuwa ikichapwa hadi ilipowasilishwa bungeni.
Hata hivyo, Lukuvi alikanusha vikali
tuhuma hizo akisema kuwa aliipata ripoti hiyo siku iliposomwa na kwamba
kama angehusika, asingekubaliwa kuwa mjumbe wa kamati ya maridhiano
iliyoundwa mwishoni mwa kikao kupendekeza maazimio ya Bunge.
“Si kweli,” alisema waziri huyo wa nchi anayehusika na sera, utaratibu na Bunge.
“Unajua PAC walikuwa wanafanya kazi
chini ya hazina. Hata Spika wa Bunge hakuiona hiyo ripoti, aliisikia tu
ikisomwa bungeni. Kwanza kamati ilikuwa ikidurufu hiyo taarifa yake eneo
la mbali na ili uipate ilikuwa ni lazima umrubuni Zitto.”
Aliongeza kusema: “Kama kweli nilikuwa
nataka kuiba taarifa yao nisingekubali kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati
ya maridhiano, iliyokutana kupitia upya mapendekezo ya PAC baada ya yale
ya awali kuzua mvutano bungeni.”
Hata hivyo, Filikunjombe, ambaye
alikuwa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, alikwenda mbali zaidi na kudai
kuwa walilazimika kumwondoa eneo la kuchapishia ripoti hiyo. “Waziri
Lukuvi alitumwa saa 9:00 usiku kuiba taarifa yetu wakati tunaichapa.
Taarifa ilikuwa katika ‘flash’ na tulipogundua hilo tulimfukuza. Sisi
tuliamua kuilinda ripoti ili isiibwe,” alisema Filikunjombe ambaye ni
mbunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM.
“Ile taarifa tuliichapa usiku wa
kuamkia Jumatano ambayo ilikuwa siku ya kuiwasilisha bungeni. Na hiyo
ndiyo ilikuwa sababu ya kikao cha Bunge kuahirishwa mara tu baada ya PAC
kuwasilisha taarifa yake, ili Serikali ikajipange,” aliongeza.
Mbali na kauli yake ya jana,
Filikunjombe aligusia suala hilo la ulinzi wakati akishukuru wabunge kwa
kushikamana katika kufikia maazimio manane ya kuwawajibisha wote
waliohusika.
Katika shukrani hizo, Filikunjombe
alisema walilazimika kukesha usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita
kuilinda ripoti yao isiibiwe na hivyo kuwashukuru watendaji wa Bunge kwa
kazi nzuri.
Hata hivyo, kabla ya kuwasilishwa kwa
ripoti hiyo kulienea taarifa kuna watu waliiiba na kunyofoa kurasa
zilizokuwa na nyaraka za vielelezo na baadaye kuanza kuzisambaza.
Polisi ilidai baadaye kuwa ilimkamata mtu aliyekuwa akisambaza vitabu hivyo vya ripoti, lakini hadi leo hajafikishwa mahakamani wala hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na polisi kuhusu maendeleo ya mtuhumiwa huyo.
Polisi ilidai baadaye kuwa ilimkamata mtu aliyekuwa akisambaza vitabu hivyo vya ripoti, lakini hadi leo hajafikishwa mahakamani wala hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na polisi kuhusu maendeleo ya mtuhumiwa huyo.
Katika sakata hilo kubwa la aina yake,
Bunge limtia hatiani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, Mwanasheria Mkuu Jaji Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati, Eliachim Maswi na wakurugenzi wa Shirika la Umeme kwa
kuhusika kwa makusudi au kwa uzembe katika kufanikisha miamala haramu
kutoka kwenye akaunti hiyo.
Bunge pia lilitaka hatua za kisheria
zishughulikie watu wote waliohusika kwenye sakata hilo, wakiwemo
wanasiasa waliopokea fedha za mgao, taasisi za kifedha zilizohusika
kufanikisha miamala haramu na wafanyabiashara waliohusika.
Vikwazo
Akizungumzia vikwazo walivyokumbana
navyo wakati wa kutekeleza majukumu yake, Filikunjombe alisema kamati
hiyo, iliyokuwa na wajumbe 24, watatu wakiwa waalikwa, kati yao 19
kutoka CCM na watano kutoka upinzani, walipata vikwazo vingi ikiwa ni
pamoja na jaribio la kurubuniwa.
Filikunjombe alisema wajumbe wa PAC
waliamua kuwa kitu kimoja na kuweka itikadi zao pembeni licha ya watu
mbalimbali kutumia fedha kutaka kuwagawa ili wasisimamie ukweli. “Unajua
sakata la Escrow linawagusa watu wenye fedha ambao walianza kuuaminisha
umma kuwa wajumbe wa PAC na sisi tumekula fedha hizo. CCM ilitakiwa
kuuchukulia wizi huu kama ajenda yake kuu,” alisema.
Alisema hakupendezwa na ushauri
uliotolewa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge kuhusu
adhabu wanazotakiwa kupewa watuhumiwa wa wizi wa fedha hizo, wakati na
yeye akiwa miongoni mwa watuhumiwa kutokana na kudaiwa kupewa Sh1.6
bilioni.
Kuhusu suala la watuhumiwa kujiuzulu,
Filikunjombe alisema siku zote Serikali haipendi kusimamiwa na Bunge,
bali inapenda kushauriwa na kwamba hiyo ndiyo sababu ya Serikali kukataa
pendekezo la PAC la wahusika kujiuzulu bila kuziomba mamlaka za uteuzi
kutekeleza hilo.
“Ukitizama suala la (mkataba wa ufuaji
umeme) Richmond si kama fedha zilichotwa wazi, lakini hili la escrow
fedha zimechotwa na waliochota wanajulikana, sasa iweje tushikwe na
kigugumizi kutaka wajiuzulu. Tena fedha hizo ni mara tatu ya zile za
Richmond,” alisema.
Zitto ataja vitisho
Kwa upande wake Zitto alisema: “Vitisho
vilikuwa vingi, lakini siyo kutoka serikalini bali kutoka kwa watu
binafsi ambao wanahusika na uchotwaji huu wa fedha.
“Mfano kupigiwa simu kuambiwa niachane
na jambo hili ama sivyo nitakufa au hata kutishiwa kuchafuliwa.
Vipeperushi vya matusi dhidi yangu vilisambazwa kwenye nyumba za wabunge
ili kuniondolea heshima na uhalali wa kuongoza vikao.”
Akieleza sababu za kuilinda ripoti,
Zitto alisema: “Kwa sababu Serikali ilikuwa inataka kuipata mapema ili
kuichakachua, hatukulala siku hiyo mpaka taarifa yetu ilipokuwa taarifa
rasmi ya Bunge. Mimi, Deo na Luhaga ndio tuliopewa jukumu hilo.”
Alisema hawakupata usumbufu kutoka serikalini, isipokuwa pale zilipoanza kujengwa hoja kuwa mahakama imezuia mjadala.
Alipoulizwa kama watuhumiwa wa sakata
hilo waliwahi kumfuata kwa namna yoyote ile alisema: “(Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Stephen) Masele peke yake ndiye alikuwa akiomba
msaada. Maswi alinipigia simu siku moja tu kuomba msaada, lakini
sikumjibu kitu. PAC tunaamini kuwa tumetenda haki kwa wananchi.”
Maswi alipopigiwa simu jana alipokea na
mwandishi alipojitambulisha, alikata simu na alipopigiwa tena kwa simu
tofauti alipokea na alipoulizwa swali hilo aliikata tena simu. Ripoti ya
PAC ilisomwa na kujadiliwa bungeni na kusababisha mtikisiko mkubwa
kutokana na mapendekezo yake kuwagusa watu wazito ndani ya Serikali.
Watu wengine waliotajwa kwenye ripoti
hiyo ni wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini
(Tanesco) na kuwavua nyadhifa zao wenyeviti watatu wa kamati za kudumu
za Bunge., Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja
(Katiba, Sheria na Utawala) na Andrew Chenge (Kamati ya Bajeti).
Mapendekezo hayo yanataka Mwambalaswa,
Ngeleja na Chenge wavuliwe nyadhifa zao, sambamba na wote waliohusika
katika muamala wa Akaunti ya Escrow kuchukuliwa hatua baada ya
uchunguzi.
0 comments:
Post a Comment