Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Mbunge wa Chato (CCM), Dk. John Magufuli (pichani), kuacha kuwabagua wananchi wa jimbo hilo kutokana na kuwachagua wenyeweviti na wajumbe wa Chadema kupitia Ukawa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka jana.
Chadema walitoa tahadhari hiyo baada ya Dk. Magufuli ambaye pia ni
Waziri wa Ujenzi, hivi karibuni kudai atapeleka fedha za Mfuko wa Jimbo
katika vijiji na vitongoji walivyoshinda wagombea wa CCM pekee.
Katibu Mwenezi wa Chadema wilayani hapa, Alex Mukama, alisema
kutokana na kauli hiyo ya Dk. Magufuli, inaonyesha wazi jinsi asivyofaa
kuendelea kuaminiwa na wananchi kwa kuwa anapingana kwa makusudi na
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayomtaka kiongozi kujiepusha
na ubaguzi wa rangi, itikadi za kisiasa, kidini na kijinsia.
Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani ya Madiwani wa Halmashauri ya
Wilaya ya Chato, Crispin Kagoma, aliwashukuru wananchi hao kwa
kudhihirisha wameichoka CCM.
Katika hatua nyingine, Chadema imewaonya wenyeviti wa vijiji na
vitongoji kupitia chama hicho kutokubaliana na maamuzi ya serikali ya
kuwasumbua wananchi kwa michango ambayo haijapitia kwenye mikutano mikuu
ya vijiji na kudhaminiwa na wananchi wenyewe.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mkuyuni, Anacret Lwegoshora (Chadema),
alisema baadhi ya viongozi wa serikali kwa kushirikiana na viongozi wa
CCM, wamekuwa wakiwashinikiza wananchi kuchangia michango pasipo
kuwashirikisha.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment