Uchaguzi wa Rais na Bunge wa Nigeria ambao awali ulikuwa ufanyike tarehe 14 Februari umesogezwa mbele na sasa utafanyika tarehe 28 ya mwezi ujao wa Machi. Kiongozi huyo wa Boko Haram ametoa vitisho hivyo baada ya kutokea milipuko miwili ya mabomu kaskazini mashariki mwa Nigeria ambapo kwa akali watu 38 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Hii ni mara ya pili kwa kamanda huyo wa Boko Haram kutoa video yenye matamshi ya kutishia kuvuruga uchaguzi wa Nigeria. Licha ya kuweko vitisho vya mara kwa mara vya Boko Haram, lakini wajuzi wa mambo wanatilia shaka kama wanamgambo hao wana uwezo na nguvu kweli za kuvuruga mwenendo wa uchaguzi mkuu ujao wa Nigeria.
Hata hivyo maafisa wa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo wamekiri kwamba, zoezi la upigaji kura halitaweza kufanyika katika baadhi ya majimbo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria kutokana na kukithiri mashambulio ya Boko Haram katika maeneo hayo.
Majimbo matatu ya Borno, Adamawa na Yobe yameandamwa zaidi na mashambulio na utegaji mabomu wa Boko Haram ikilinganishwa na maeneo mengine na hadi sasa yangali yanakabiliwa na mashambulio ya wanamgambo hao wa kitakfiri.
Mwezi Januari uliopita, ulishuhudia kushadidi mashambulio ya Boko Haram katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria, ambayo yalivuka mpaka na kuingia pia katika maeneo ya nchi jirani kama Cameroon, Chad na Niger.
Kushadidi mashambulio hayo kumeweka wazi ukweli kwamba, Boko Haram ndiyo tishio kuu la amani na usalama wa nchi za eneo hilo. Kwa muktadha huo tishio la Abubakar Shekau la kuvuruga uchaguzi wa Nigeria ni dogo ikilinganishwa na hatari yenyewe ya kundi hilo la kigaidi.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kusogezwa mbele zoezi la uchaguzi wa Nigeria na kujitoa Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo katika chama tawala cha People's Democratic (PDP) ni mambo ambayo yanaweza kuwa na taathira kwa matokeo ya uchaguzi huo wa Machi 28.
Obasanjo ambaye aliwahi kuhudumu kama jenerali jeshini, aliliongoza taifa la Nigeria akiwa Rais mwaka 1999 hadi 2007.
Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba, kujiengua Obasanjo kutoka chama tawala ni pigo kubwa kwa chama hicho katika uchaguzi ujao.
Obasanjo baada ya kumaliza mihula yake miwili kama Rais aliendelea kuwa mwenyekiti wa chama tawala cha PDP ambapo ushawishi na heshima yake ya kisiasa ni mambo ambayo yanaelezwa kuwa yalikuwa na nafasi muhimu katika kukipatia ushindi mara mbili mtawalia chama tawala katika uchaguzi wa Rais na Bunge.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kujiengua jenerali huyo wa zamani wa jeshi kutoka katika chama tawala kunaamnisha kusita himaya na uungaji mkono wake kwa mgombea wa chama tawala katika uchaguzi wa mwezi ujao.
\
Wataalamu wa mambo wanaamini kuwa, ukosoaji wa mara kwa mara wa Obasanjo kwa serikali ya Nigeria kutokana na kushindwa kulitokomeza kundi la Boko Haram, kuongezeka ufisadi serikalini na kudorora uchumi wa nchi kulikosababishwa na kuporomoka bei ya mafuta katika soko la dunia kutamsaidia mgombea wa upinzani Muhammadu Buhari katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa mwezi ujao nchini Nigeria.
Hata hivyo Obasanjo amesisitiza kwamba, hatamuunga mkono Buhari katika kampeni zake za uchaguzi. Pamoja na hayo, wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kitendo tu cha Obasanjo kujitoa katika chama tawala kitampiga jeki Buhari katika uchaguzi ujao.
Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, kuanzia sasa Muhammadu Buhari ameandaliwa uwanja wa kujipatia kwa urahisi ushindi katika uchaguzi ujao ambapo anachuana na Rais Goodluck Jonathan anayeandamwa kwa ukosoaji mkubwa. Hata hivyo mambo yatakuwa hivyo, iwapo jeshi la Nigeria na vikosi vya kieneo havitafanikiwa kulisambaratisha na kulitokomeza kundi la Boko Haram kabla ya uchaguzi huo wa mwezi Machi.
0 comments:
Post a Comment