Dodoma. Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi leo umemtangaza Dk John Magufuli kuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Dk Magufuli amepata asilimia 87 ya kura zote za wajumbe, huku wengine walioingia tatu bora; Balozi Amina Salum Ali akipata asilimia 10.5 na Dk Asha Rose Migiro akipata asilimia 2.4.
Mkutano Mkuu ulipiga kura jana usiku chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Dk Magufuli alifanikiwa kufika katika hatua ya tatu bora akiwa na watangaza nia wengine; Dk Asha Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali.
Watatu hao walifanikiwa kuingia hatua hiyo ya mwisho ya kupigiwa kura na mkutano mkuu baada ya kuwabwaga makada wengine wawili, Bernard Membe, ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa kutokana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuenguliwa na Kamati Kuu juzi, na January Makamba katika kura zilizopigwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu.
Awali kabla ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu jana, Kikwete aliwataka wajumbe kumuunga mkono mgombea atakayepitishwa kupeperusha bendera ya chama hicho na kuachana na makundi.
“Wagombea wapo watatu na wote wana sifa za kuwa Rais. Halmashauri Kuu imewapitisha kwa kujiridhisha na tabia na mienendo yao na atakayepitishwa ataiongoza nchi yetu vizuri. Anatakiwa apatikane Rais zaidi yangu ili tusonge mbele. Tunataka rais atakayefanya mambo zaidi yangu,” alisema JK.
“Tumevuka hatua ya makundi na sasa tunatafuta mgombea wa chama na si mgombea wa kundi au mgombea binafsi. Wagombea urais waliojitokeza walikuwa 38 na makundi lazima yalikuwa mengi. Tukipata mgombea mmoja makundi yanatakiwa kuyeyuka.”
Hisia za wajumbe kwa Dk Magufuli zilionekana wazi wakati makada hao walipopewa dakika 15 za kujieleza mbele ya Mkutano Mkuu, huku mwenyekiti akiweka sharti la kuzuia kushangilia hata kama wakiguswa. Lakini sharti hilo lilionekana kuwasumbua wajumbe hao na mara kwa mara wakajikuta wakilipuka na kushangilia.
John Pombe Magufuli
Akijinadi kwenye mkutano huo, Dk Magufuli, ambaye alizungumza kwa dakika tisa kuanzia saa 5:55 hadi saa 6:04 usiku, aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo, wakiwamo wageni waalikwa na muda huo wajumbe wakaanza kumshangilia.
“Naombeni kura kwa sababu ninaamini kuwa nitafanya kazi na nyinyi na mtanituma na nitakuwa mwakilishi wenu na nitailinda CCM katika kushinda kikamilifu na kushika dola ili kuiongoza nchi hii. Nitadumisha Muungano wetu,” alisema Magufuli.
Chanzo: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment