• Yanga robo-fainali Kagame

    KIKOSI CHA YANGA

    Malimi Busungu alifunga goli lake la tatu katika mechi tatu za Yanga za Kombe la Kagame la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati na kuisaidia timu hiyo kuingia robo-fainali licha ya kupoteza mchezo wa kwanza, baada ya jana kuifunga KMKM 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa.

    Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi sita baada ya mechi tatu na kushika nafasi ya tatu kwenye Kundi A ambalo timu tatu za kwanza zinaingia robo-fainali.

    KMKM imeaga ikiwa na pointi tatu wakati Telecom imebakiza mchezo mmoja ikiwa kapa mpaka sasa. 

    Al Khartoum na Gor Mahia zina pointi saba kila moja baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa awali wa michuano hiyo kwenye uwanja huo jana, Wasudan hao wakiongoza kwa kuwa na uwiano mkubwa wa magoli (6) kulinganisha na Wakenya (3).

    Ilielekea kama siku nyingine mbaya uwanjani kwa Yanga iliyolazwa 2-1 na Gor Jumamosi kwa muda mrefu wa mchezo wa jana mpaka Busungu, ambaye alifunga magoli mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Telecom katikati ya wiki, alipobadili uelekeo wa upepo.

    Busungu akiwa amepokea pasi ya Deus Kaseke kutoka upande wa kulia ndani ya eneo la hatari katika dakika ya 56, aliachia shuti la mguu wa kulia ambalo lilimbabatiza beki kabla ya kupiga mpira huo kwa mara ya pili kumzunguka Nassor Abdullah langoni mwa KMKM.

    Mbali na bao hilo la Busungu aliyejiunga na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Bara akitokea Mgambo JKT, jahazi la KMKM lilizama kabisa kufuatia goli la kujifunga la beki Said Athuman katika robo ya mwisho ya mchezo huo wa Kundi A.

    Akiwa anawania mpira wa juu kwa pamoja na Amisi Tambwe aliyeingia kutoka benchini, Athuman alijaribu kumrudishia kwa kichwa mlinda mlango Abdullah langoni lakini mpira huo ukaishia kutumbukia wavuni karibu na mlingoti wa goli.

    Yanga ingeweza kwenda mapumziko ikiongoza lakini Donald Ngoma ambaye jana alirudi uwanjani baada ya kusimama mechi moja tangu apewe kadi nyekundu katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Gor Jumamosi iliyopita, na Godfrey Mwashiuya walipoteza nafasi nzuri mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

    Wakati Ngoma alishindwa kutumia vizuri krosi ya Deus Kaseke katika dakika ya 38 na kupiga mpira nje, shuti la Mwashiuya kutoka ndani ya eneo la hatari dakika sita baadaye lilipanguliwa na Abdullah langoni mwa KMKM kabla ya kuoshwa na mabeki.

    Timu zilikuwa:
    KMKM: Nassor Abdullah, Khamis Ali Khamis, Tizo Chrles Chomba, Said Idrisa Said, Mussa Said Athuman, Mateo Simon, Juma Mbwana Faki, Haji Simba Salim, Ibrahim Khamis Khatib, Nassor Ali Omar.

    YANGA: Ally Mustapha 'Barthez', Nadir Haroub 'Canavaro', Mbuyu Twite (Andrey Coutinho dk.90), Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Malimi Busungu (Amis Tambwe dk.60), Deus Kaseke, Goefrey Mwashiuya, Juma Abdul (Joseph Zuttah dk.85).

  • 0 comments:

    Post a Comment

    GET A FREE QUOTE NOW

    Lorem ipsum dolor sit amet, consectetuer adipiscing elit, sed diam nonummy nibh euismod tincidunt ut laoreet dolore magna aliquam erat volutpat.