Lowassa, ambaye ameshika nafasi ya pili katika mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano akiweka rekodi ya kukusanya kura milioni 6.07 ambayo ni rekodi kwa mgombea wa upinzani, alitoa kauli hiyo jana mchana katika hafla ya chakula cha mchana ya kuishukuru timu yake ya kampeni iliyofanyika Kawe, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa, wanahabari na familia yake.
“Nimefarijika sana, asanteni kwa msaada mlionipa, sina cha kuwalipa,” alisema waziri huyo mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne aliyeihama CCM na kujiunga na Chadema mwezi Julai.
“Ukweli ni kwamba kila mmoja alifanya kazi yake. Tujiandae kwa awamu ya pili na safari ndiyo imeanza,” alisema na kushangiliwa.
“Unaweza kuchelewesha bahati ya mtu, lakini hauwezi kuiondoa,” aliongeza. Hata hivyo, Lowassa hakueleza awamu ya pili itahusisha mambo gani. Tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, Lowassa amezungumza na vyombo vya habari mara mbili, mara ya mwisho akieleza jinsi alivyowasilisha pingamizi lenye hoja tatu kuhusu mwenendo wa uchaguzi kwa mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva ambalo liligonga mwamba.
Katika tamko lake, Lowassa alikuwa akipinga matokeo ya kura za urais yaliyokuwa yakitangazwa na NEC akidai kuwa si halisi na kuitaka isitishe kutangaza, lakini tume hiyo haikueleza lolote na badala yake iliendelea kutangaza matokeo ya majimbo na baadaye mshindi wa urais.
Mambo hayo matatu yaliyowasilishwa NEC ni kupunguzwa kwa kura zake, kuongezewa kura kwa mgombea wa CCM na kutangazwa matokeo batili kwa wagombea wa Ukawa.
Lowassa aliyeanza kwa kuwatambulisha watu wake wa karibu waliomshauri masuala muhimu na nyeti katika kampeni, akiwemo waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, alizungumza kwa kifupi, akitoa mfano wa jinsi majeshi ya ukombozi wa nchi mbalimbali barani Afrika yalivyorudi nyuma kujipanga baada ya kushindwa.
Muda mfupi kabla ya Lowassa kueleza hayo, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliufananisha Uchaguzi Mkuu na vita, akisema kulikuwa na njama za makusudi za kuhakikisha Lowassa hapati ushindi.
Alisema wagombea ubunge kutoka vyama vinavyounda Ukawa vya NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF, waliibiwa kura na ushindi kupewa wagombea wa CCM.
Mbowe alisema kwa kuwa hawawezi kupinga matokeo ya urais mahakamani, watafungua kesi za kupinga matokeo ya ubunge.
“Tunachofanya, tunarudi nyuma, tunajipanga kukata rufaa kupinga matokeo katika majimbo zaidi ya 30,” alisema Mbowe.
“Wagombea wetu waliokuwa wabishi na kupigana kwelikweli walitangazwa washindi, lakini kuna majimbo ambayo wagombea wetu waliporwa ushindi waziwazi kabisa. Kwa kuwa ubunge unapingwa mahakamani tutafanya hivyo,” alisema Mbowe.
Miongoni mwa majimbo ambayo matokeo yake yalikuwa na ubishi ni Nyamagana, ambako mbunge maarufu wa Chadema, Ezekiah Wenje alishindwa na mgombea wa CCM,Stanslaus Mabula baada ya mvutano uliochukua muda mrefu. Pia mbunge wa NCCR Mageuzi, David Kafulila wa Kigoma Kusini aliangushwa baada ya matokeo kuibua mzozo mkali uliosababisha polisi kuingilia kati.
Mbowe pia alisema kuwa wanahamishia nguvu Zanzibar kuungana na mgombea urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad kudai haki yake.
Mbowe alisema kitendo cha kufutwa kwa uchaguzi huo kina mkanganyiko mkubwa na kusisitiza kuwa kuanzia wiki ijayo Ukawa itapiga kambi kwenye visiwa hivyo kuhakikisha haki inatendeka.
Baadhi ya viongozi wa Ukawa waliohudhuria hafla hiyo ni makamu mwenyekiti wa Chadema –Bara, Profesa Abdallah Safari, mwenyekiti wa NCCR na mbunge mteule wa Vunjo, James Mbatia na kaimu katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu.
-Mwananchi
-Mwananchi
0 comments:
Post a Comment