Uliyafahamu haya kumhusu Salim Kikeke? Ni mtangazaji mashuhuri wa shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC). |
Baada ya kumaliza Stashahada ya Umwagiliaji katika Chuo cha Kilimo
Nyegezi, Mwanza, alikutana na changamoto kadhaa hasa ya kukosa ajira kwa
kipindi cha zaidi ya miaka mitatu mfululizo.
”Nilimaliza Stashahada
yangu mwaka 1994 kozi ya Umwagiliaji, kwa sasa labda ningekuwa bwana
shamba au mfanyakazi wa kilimo,” anasema Kikeke.
Baada ya kumaliza chuo,
juhudi za kusaka ajira zilikuwa ngumu.
Kwa karibu mwaka mzima wa 1995,
alikwenda katika machimbo ya Tanzanite ya Mererani Arusha
“Hakukuwa na
ajira na kishawishi cha kujiingiza katika uhalifu kilikuwa kikubwa,”
anasema bila kueleza zaidi.
Katika hatua ya kuepuka mazingira hayo
aliamua kuwa ‘Mwanaapolo’ kama wanavyojulikana wachimbaji wa Tanzanite
yaani kutumika kuingia kwenye mashimo kubeba mizigo au kazi nyingine
migodini.
Baada ya kushauriwa na mama yake kuondoka mchimboni, alirejea
Dar es Salaam.
Katika kipindi hicho Kikeke anasema alikuwa akishinda
kijiweni mitaa ya Sinza Kumekucha akiwa na rafiki yake,
Joseph
Mboya ambaye kwa sasa ni marehemu.
Mara baada ya kuona matumaini
yakififia kupitia taaluma yake ya kilimo, Kikeke aliamua kubadilisha
ukurasa wa maisha baada ya kupiga hodi katika ofisi za kituo cha TV cha
CTN ambacho kilikuwa na redio wakati huo ikijulikana kama Classic FM
ambayo kwa sasa ni Magic FM.
Sababu, nia na ujasiri wa kuchukua uamuzi
huo, haikutokea kama ajali, bali ilitokana na ushawishi aliokuwa
ameupata kutoka kwa mama yake mzazi ambaye ni marehemu kwa sasa.
“Mama
yangu alikuwa wa kwanza kunijengea uwezo wa kuingia katika utangazaji,
alikuwa anapenda sana kusikiliza habari za redioni na alinishawishi
kufuatilia kila habari iliyokuwa inaendelea duniani, nikawa na uwezo wa
kutamka maneno vizuri na kusoma habari,” anasema Kikeke.
Ilikuwa ni
mwishoni mwa 1997, Kikeke alifika katika ofisi za kituo cha kurusha
matangazo cha CTN.
“Kwa sasa wanaita Magic FM, walikuwa wanafungua kituo
kipya cha Classic FM hivyo niliomba kufanya kazi bure, nikapewa kipindi
cha kucheza miziki ya Kiingereza,” anasema Kikeke
Jambo la kujifunza
hapa ni kwamba wakati mwingine katika kusaka ajira, kubali kufanya kazi
bila ya malipo, onyesha jitihada zako, huenda ikawa ni njia nzuri ya
kuajiriwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo yale ambayo huenda mtu
amekwenda kwa ajili ya masomo kwa vitendo.
Njia sahihi ya kukaa katika
ajira usiyo na ujuzi nayo Anasema baada ya kupata uhakika wa kuendelea
na kazi hiyo, Januari mwaka 1998, Kikeke aliamua kwenda kusoma kozi fupi
ya Utangazaji habari katika chuo cha uandishi wa habari cha ‘Tanzania
School of Journalism (TSJ)’.
”Pale nilisoma cheti kwa miezi mitatu na
kurudi tena kazini, nikaanza kusoma habari za kiingereza na Kiswahili
wakati mwingine nilikuwa naenda kutafuta habari,” anasema Kikeke.
“Hata
hivyo mwezi mmoja baadaye wakanifukuza kazi kwa sababu ambazo
nisingependa kufafanua zaidi,” anasema.
Wakati mwingine hata baya lina
uzuri wake Kikeke baada ya kufukuzwa kazi, hakuishia kulia mtaani,
badala yake alianzisha mkakati wa kusaka ajira tena kwenye taasisi yenye
hadhi ya juu zaidi, Radio Tanzania (RTD) ambayo sasa ni Shirika la
Utangazaji Tanzania (TBC), hiyo ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 1998.
”Kwa
kipindi hicho Abdul Ngarawa alikuwa mkurugenzi wa RTD, nikapelekwa
idhaa ya Kiingereza, ‘English Service’, na kuandaa vipindi vya muziki
kila siku kuanzia saa 12:00 jioni mpaka saa 6:00 usiku,” anasema Kikeke
na kufafanua kuwa alikuwa akifanya kazi kwa muda ‘part-time.
Alianza
kupangiwa vipindi vya kutangaza baada ya kukaa kwa zaidi ya mwaka mmoja.
“Baadaye nikapewa kipindi cha Mwelekeo kilichoanzishwa wakati wa
maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, nilikuwa mtangazaji
wa mwanzoni kabisa katika kipindi hicho,” anasema Kikeke.
Katika kipindi
hicho, Radio Tanzania walianzisha kituo cha matangazo cha FM, kiitwacho
PRT kikitoa matangazo kwa lugha ya Kiingereza.
RTD na Kituo cha PRT
ndizo kwa sasa zinafahamika kama TBC na TBC1.
“Mimi nikaondoka pale na
kurudi tena CTN,” anasema.
Kurudi CTN Baada ya kurudi katika kituo
hicho, Kikeke alifanikiwa kupata nafasi ya kusoma habari kwenye TV mpaka
mwezi Agosti wakati kampuni hiyo ilipouzwa na kuwa chini ya kituo cha
Channel Ten na DTV. Baadae alihamia ITV.
Kuingia ITV/Radio One. Baada ya
hapo alifanikiwa kuandika barua ya maombi ya kazi katika Kituo cha
Radio One.
“Kwa wakati huo Charles Hilary ndiye alikuwa Mkuu wa Kitengo
cha Radio One, akaniomba nimpatie mfano (Demo) ya kipindi chochote
nilichowahi kufanya, kwa bahati mbaya sikuwa na ya radio ila nikawa na
ya TV”, anasema Kikeke.
Anaongeza kuwa hali hiyo ikamfanya abadilishe
mlango wa kutoka Redio One na kuingia ITV.
“Charles Hilary akaipeleka
ile demo upande wa televisheni ya ITV, kulikuwa na Betty Mkwasa na Joyce
Mhaville, wakaipenda kazi yangu na kuagiza niripoti pale kazini,”
anasema.
Kikeke alipangiwa jukumu la utangazaji wa vipindi vya taarifa
za habari kila siku na habari za ‘Jiji Letu’ hata hivyo mambo
yalibadilika kwa muda mfupi pale ofisini.
Radio One walikuwa ni Redio
washirika wa BBC hivyo walikuwa na mkataba wa kuchukua mtangazaji mmoja
kila mwaka na kumpeleka kufanya kazi makao makuu ya BBC kwa muda wa
miezi kadhaa.
Anasema Mwezi Mei 2003 nikafaulu majaribio ya kuingia BBC,
ambako anaendelea hadi leo.
Kikeke ni mtoto wa pili kati ya watoto
watatu.
Ni baba wa mtoto mmoja ambaye anasoma darasa la saba nchini.
“Huku London ninaishi peke yangu,” anasema.
0 comments:
Post a Comment