• UBINGWA WA EPL LIVERPOOL: BORA NIKISUBIRI KITABU CHA STEVEN GERRARD

    Tarehe 27/04/2014, moja ya tarehe mbaya kabisa kwa mashabiki wa Liverpool, moja ya tarehe ambazo zitadumu vichwani mwao, moja ya tarehe ambayo kwa namna moja ama nyingine ndio iliyochochea kipenzi Chao kuondoka Luis Suarez, moja ya tarehe ambayo inaweza kuwa ndio ilifuta na imefuta matumaini ya Brendan Rodgers kuwa kocha wa kwanza kuipa furaha Liverpool. 
     
    Ndio ni moja ya tarehe ambayo aliyeyasababisha yote haya ni mtu anayelaumiwa ndani ya moyo. 

    Ni tarehe ambayo machozi yalichuruzika ndani ya mioyo ya mashabiki wa Liverpool na sio nje.

     Kipenzi Chao, mpiganaji wao, mwanajeshi wao, ndugu yao, mtoto wao na kijana wao Steven Gerrard alipeperusha mwenyewe ndoto aliyokuwa anaisubiri kwa muda mrefu, aliangusha pensheni iliyokuwa imekaribia kutua mikononi mwake.


    Katika miaka ambayo alikuwa na nguvu ya faru hakuwahi kuipata bahati hii, bahati ilikuja akiwa na nguvu ya Digi Digi Tu. 

    Nguvu ya kusambaza mipira akiwa mbele kidogo ya sehemu ya ulinzi, wakati kazi kule mbele ikiwa inafanywa na wengine. 

    Bahati mbaya akateleza akiwa  kapasiwa mpira mbele ya adui, mwafrika wa Senegal, Demba Ba akafunga moja ya magoli rahisi kabisa kuwahi kuamua hatma ya ubingwa wa Ligi kuu ya England.

    Kwa kazi ndogo Ba akabaki kuwa mchezaji atakayekumbukwa sana kwa kuwaliza Liverpool. 

    Baada ya goli sura ya Gerrard ilishajaa wasiwasi, haikuwa ile ya Instabul walipokuwa wamefungwa 3 – 0 na AC Milan, hii ilikuwa tofauti,wakati kule alirekebisha makosa ya wengine akiwa na nguvu hapa alitegemea wengine warekebishe yake huku akiwa hana nguvu, jambo lililofanana ni kwamba kwa nyakati zote yeye ndio alikuwa nahodha.

    Kuna muigizaji wa Marekani aitwaye Orson Welles aliwahi kusema kuwa “Nobody Gets Justice. People Only Get Good Luck Or Bad Luck”, alimaanisha hakuna ambaye hupata kile anachostahiki,watu hupata bahati nzuri au bahati mabaya tu. 

     Kama kuna mtu anaweza kuamini katika bahati kama Orson Welles basi ni Steven Gerrard.

     Kama kuna watu wanaamini ulimwengu huu una maisha ya bahati basi ni huyu Steven Gerrard, wakati akicheza soka katika kiwango cha kustua, wakati Dunia ikishangilia magoli yake ya guu la kulia ya kusisimua bado anabaki kuwa moja ya wachezaji bora kabisa kutokuwahi kushinda taji la Ligi kuu ya Uingereza.

    Javier Mascherano na Xabi Alonso
    Javier Mascherano na Xabi Alonso
    Kama kuna kitu kinamtafuna Steven Gerrard basi naamini ni Uzalendo ile hali ya kuwa ‘Mfalme Anfield’, kitendo cha kuwa mchezaji anayeimbwa zaidi pale Anfield, kitendo cha kutajwa kuwa mchezaji aliyeistua zaidi “KOP”  pengine na kuishi maisha ya kumuenzi mpwa wake JON PAUL GILHOOLEY.

     Naamini kuna wakati Steve anamtizama Alonso kisha anacheka badala ya kulia, anamtizama Mascherano kisha anakipiga kifua chake, ndio hawa walishindwa kushinda Ligi Kuu ya Uingereza wakaenda kushinda huko kwingine anaweza kuamini hata yeye angeenda huko nje angeweza sana.

    Tatizo linakuja hapa, Lampard, Scholes na yeye mwenyewe. Viungo bora kabisa kuwahi kutokea, viungo bora kabisa waliopata kuvaa jezi ya ‘Simba Watatu’ pamoja lakini bado hawa chumba chao kina kitu cha zaidi kuliko Steven Gerrard, medani ya EPL. 

    Medani ambayo hata Macheda ameitunza.  Mwaka 2009 Zinedine Zidane aliwahi kusema kwamba Steven Gerrard ndiye alikuwa mchezaji bora Zaidi duniani, hapa ndipo Dunia inakosa haki kama maneno ya Orson Welles, wakati Tom Cleverley na Jack Rodwell pia na Scott Sinclair wakiwa na Medani, Gerrard hajawahi kuvaa na sifikirii kama anaweza kuivaa ingawa naamini anaitamani sana. 

    Hata wale mashabiki wa Kop END jukwaa maarufu sana pale Anfield wanahitaji ubingwa kwanza kwa ajili yake huyu kabla ya wao wenyewe.

    Gerrard ana miaka 34 sasa, sio muda mrefu ataanza kuwa anacheza dakika 45 tu au 50 kila baada ya mechi moja, sio muda mrefu tutaanza kushuhudia ufalme wa kina Raheem Sterling huku yeye akiwa benchi pale Anfield, inatia huzuni sana.

    Kipindi hicho akili ya kuupumzisha mwili itakuwa inamjia kichwani, dili za skysports zitakuwa zinamnukia, na kitabu chake kitakuwa kinakaribia kutoka pia. 

    Najiuliza tu kurasa ngapi za kitabu chake zinaweza kuwa na maneno ya kukutoa machozi, kuna kurasa kadhaa zitaelezea ukame wa hilo Kombe Liverpool, kuna kurasa kadhaa zitakuelezea kifo cha binamu yake katika Hillsborough, kuna kurasa kadhaa zitakuonyesha picha nzima ya alivyoteleza pale Anfield, bahati mbaya kwa Gerrard katika hilo tukio sio Drogba atakayetajwa au Wayne Rooney bali ni Demba Ba.

    Unajua mashabiki wa Liverpool watakimbilia kurasa zipi? Zile zitakazolelezea ROAD TO INSTABUL, yaani safari ya Instabul. 

    Watacheka kuona maneno ya Gerrard aliyowaambia wenzie wakati wanarudi uwanjani dhidi ya AC Milan, wataishia katika magoli ya Suarez, kile kipande cha utelezi watakiruka.

     Usijiulize sana, hata sisi wanadamu tunaamini kama Orson Welles, tunajifanya kuamini katika bahati mbaya hata kama tumedhurika, hata Gerrard analindwa na hili, historia yake inamlinda, uzalendo wake unambeba, najaribu kujiuliza kama angeteleza KOLO TOURE mambo yangekuwaje.


    Kila nikitizama muelekeo wa ligi kuu Uingereza sioni uelekeo wa Liverpool kama msimu uliopita, naiona mipango ya Gerrard ikiendelea kuwa ndoto. Mwandishi wa Marekani Gloria Steinem aliwahi kusema “dreaming is after all the form of planning” yaani ndoto nayo ni namna ya kupanga. Hapa ndipo Gerrard alipo anapanga kichwani, ndotoni anashinda lakini uwanjani miaka inaenda.

     Inawezekana Liverpool ikashinda ubingwa kabla hajastaafu lakini bado haitokuwa kwa sababu yake, ndio maana mi nimeamua kukaa kukisubiri kitabu chake badala ya yeye kushinda ubingwa, ikitokea atashangilia lakini haitokuwa kama ambavyo ingekuwa msimu uliopita, hatolia kama ambavyo alianza kulia msimu uiopita, ndo maana naamini kitabu chake kitakuwa na hisia kuliko kombe lake, wacha nikisubiri. 

    Ahsanteni.by Nicasius Coutinho Suso

    mkala na ;Shafih Dauda

  • 0 comments:

    Post a Comment

    GET A FREE QUOTE NOW

    Lorem ipsum dolor sit amet, consectetuer adipiscing elit, sed diam nonummy nibh euismod tincidunt ut laoreet dolore magna aliquam erat volutpat.