Rais Jakaya Kikwete amemteua Prof.Mussa Juma Assad kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) |
Kituo cha ITV kimeripoti kuhusu taarifa
ya uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) Tanzania, hapa
nimekuwekea taarifa rasmi kutoka kwenye Website ya Ikulu Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Profesa Mussa Juma
Assad kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu,
Desemba Mosi, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, inasema
kuwa uteuzi wa Bwana Assad ulianza Novemba 5, mwaka huu, 2014.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Bwana Assad ataapishwa kesho, Jumanne, Desemba 2, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.
Kabla ya uteuzi wake, Bwana Assad
alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
na anachukua nafasi ya Bwana Ludovick Utouh ambaye amestaafu kwa mujibu
wa Sheria za Utumishi wa Umma.
Profesa Assad ni msomi, mwenye
weledi, ujuzi na uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha ambaye
ana Shahada ya Uzamivu wa Uhasibu (PHD in Accounting) kutoka Chuo Kikuu
cha Southampton, Uingereza mwaka 2001 na Shahada ya Uzamivu katika
Udhibiti wa Fedha (MA in Financial Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha
Dublin City, Jamhuri ya Ireland mwaka 1991.
Profesa Assad pia ana Stashahada ya
Kitaaluma ya Uhasibu (Professional Diploma in Accounting) kutoka Chuo
Kikuu cha Dublin City mwaka 1990 na Shahada ya Biashara (Bachelor of
Commerce) ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mwaka 1988.
Pamoja na uzoefu wa kitaaluma,
Profesa Assad anao uzoefu mkubwa katika eneo la uhasibu na ukaguzi.
Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) kwa miaka saba
(2007 – 2014); ni Rais na Mjumbe wa Chama cha Wahasibu Afrika (Pan
African Federation of Accountants) tangu mwaka 2012; na ni mjumbe wa
Bodi kadhaa za Wakurugenzi nchini Tanzania.
Katika kumteua Profesa Mussa Juma
ASSAD kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Rais anayo
imani kubwa kuwa elimu, weledi, ujuzi na uzoefu ambao Profesa Assad anao
utamwezesha kutekeleza vema majukumu ya nafasi hiyo muhimu sana katika
utawala bora wa nchi yetu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
1 Desemba,2014
Kupitia Mtandao wa Twitter ITV iliandika hivi; “… #Habari Rais Jakaya Kikwete amemteua Prof.Mussa Juma Assad kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)…”– ITV@ITVTANZANIA